Utawala

Ikiwa usimamizi ndio kile kinachofanywa, katika mazingira fulani, ili kufikia matokeo yanayotazamiwa kulingana na njia na rasilimali zilizopo, utawala unahusu nani anaamua kuhusu shughuli za usimamizi (na raslimali – watu na fedha), jinsi maamuzi hayo yanavyochukuliwa, na kama hatimaye yametekelezwa (ambayo ni pamoja na kuhakikisha kuwa rasilimali zinazotakiwa na za kutosha zinapatikana).

Utawala umetafsiriwa zaidi kama mchakato wa “mwingiliano kati ya miundo, michakato na mila ambayo huamua jinsi mamlaka na majukumu yanavyotekelezwa, jinsi maamuzi yanavyofanywa na jinsi raia au wadau wengine wanavyokuwa na maoni yao”.[1] Kiuhalisia, kwa eneo fulani, utawala unahusu “kushikilia mamlaka na wajibu na kuwajibika kwa maamuzi muhimu kulingana na njia za kisheria, kimila au vinginevyo halali” [2]. Ni kuhusu “kuchukua maamuzi na kuhakikisha masharti ya utekelezaji wake kwa ufanisi”, yaani, “mchakato wa kuendeleza na kutekeleza mamlaka na wajibu kwa muda, ikiwa ni pamoja na kuhusiana na michakato ya kujifunza na taasisi zinazobadilika katika jamii”.[3]

Utawala labda ndio kipengele muhimu zaidi kinachohitajika kutafsiri maeneo ya hifadhi za jadi za Kongani. Badala ya kutegemea kikamilifu haki za kumiliki mali na hatimiliki (ambazo ni muhimu lakini si muhimu sana), maeneo ya hifadhi za jadi yamejikita katika uwezo na utashi bora wa watu wa asili na jamii nyingine kutawala maeneo yao. Katika maeneo ya hifadhi ya jadi ya Kongani — tunapata watu wa asili na jamii ambazo, kupitia #taasisi zao za utawala, hufanya (au kujitahidi) kufanya maamuzi, kutekeleza sheria zao za kufikia na kutumia, malengo, kujifunza, kushirikisha, kuishi na kujumuisha tunu zao wenyewe na hisia ya utambulisho kuhusiana na asili, wanadamu wengine na viumbe vingine vya kidini (zaidi ya-binadamu).

Mkataba kuhusu Bioanuwai na Umoja wa Uhifadhi wa Mazingira Kimataifa zinatofautisha aina nne pana za utawala kwa maeneo yaliyohifadhiwa (angalia #Eneo Lililohifadhiwa) kulingana na jinsi ambavyo wahusika wana mamlaka makubwa na wajibu wa kufanya na kutekeleza maamuzi. Aina hizo ni: (A) utawala wa serikali (kama kwenye hifadhi ya taifa ya kawaida, inayoendeshwa na wakala wa serikali); (B) utawala wa uwanda ambapo wadau mbalimbali kwa pamoja (kwa mfano, kwa mazingira yaliyohifadhiwa, ambapo maamuzi hufanywa na bodi inayojumuisha wizara za kimataifa, manispaa za mitaa, vyuo vikuu na asasi zisizo za kiserikali za uhifadhi); (C) utawala wa watu binafsi au mashirika (kwa mfano, eneo la binafsi lililohifadhiwa, ambapo maamuzi yanafanywa na wamiliki wa ardhi); na (D) utawala wa jamii ya asili na/au jamii za wenyeji (kwa mfano, eneo la huifadhi ya jadi kwa Kongani, ambapo maamuzi hufanywa na watu au jamii husika). Kutambulika kwa aina mahususi ya utawala wa pamoja wa watu wa asili na jamii za wenyeji katika sera ya kimataifa ya uhifadhi ni muhimu sana, kwa sababu inatoa heshima kwa jukumu lao muhimu katika kuhifadhi raslimali za asili na kudumisha bioanuwai kwenye sayari yetu – pamoja na manufaa kwa wanadamu wote.

Kufaa’ kwa aina fulani ya utawala kunategemea historia ya umiliki na haki za kila eneo, na vilevile katika hali ya mahusiano kulingana na mahali na shughuli za kujitawala kwa uendelevu kwa jamii zao zinazoweza kuwa za wamiliki. Kama ilivyokumbushwa katika miongozo ya hiari iliyopitishwa na nchi Wanachama wa Mkataba kuhusu Bioanuwai mwaka 2018, aina hiyo ya utawala inapaswa “kulenga muktadha mahususi, unaojumuisha jamii, onaoheshimu haki, na yenye ufanisi katika kutoa matokeo ya uhifadhi na kipato cha kujikimu”. [4]

Katika miongo kadhaa iliyopita, Umoja wa Uhifadhi wa Mazingira Kimataifa na nchi Wanachama wa Mkataba kuhusu Bioanuwai wameongeza utambuzi wao wa “tunu zenye vipengele vingi vya utawala wa pamoja wa watu wa asili na jamii za wenyeji” [5] na kubainisha kanuni na tunu za ‘utawala bora’ zinazopaswa kuheshimiwa na kukuzwa. Hizi ni pamoja na: “taratibu na mifumo inayofaa: kwa ushiriki kikamili na wenye ufanisi wa watu wa asili na jamii za wenyeji; kwa ushiriki wenye ufanisi wa na/au uratibu na wadau wengine; kwa ajili ya (kutambua na kuupokea) umiliki wa kimila na mifumo ya utawala; kwa uwazi na uwajibikaji; kwa ugawaji sawa wa faida na gharama, (na kwa) kuzingatia vifungu vya 8(j) na 10(c) (za Mkataba kuhusu Bioanuwai) na masharti, kanuni na miongozo inayohusiana” [6]. Kwa maneno mengine, maamuzi kuhusu maeneo yaliyohifadhiwa yanapaswa kufanywa na kutekelezwa “kihalali, kwa ustadi, kwa ujumuisho, kwa haki, kwa maono, kwa kuwajibika na huku ukiheshimu haki”.[7]

Kulingana na Kituo cha Utawala wa Watu wa Asili, [8] kuna nguzo tano za utawala wenye ufanisi (na kuna uwezekano unafaa): 1. Watu (maono ya pamoja ya kimkakati, kushirikishana taarifa muhimu na kushiriki katika kufanya maamuzi); 2. Ardhi (uadilifu wa eneo, kukuza uchumi, heshima kama roho ya nchi); 3. Sheria na mamlaka (upanuzi wa mamlaka na utawala wa sheria); 4. Taasisi (uwiano wa kitamaduni wa taasisi na uhusiano mzuri wenye ufanisi kati ya serikali, mashirika yanayosimamia matokeo, uwazi na haki); na 5. Rasilimali (uwezo wa rasilimali watu, usimamizi wa fedha, tathmini ya utendaji, uwajibikaji na utoaji taarifa, na aina mbalimbali za vyanzo vya mapato).

Ni zipi aina za utawala?

Tunazungumza juu ya aina mbalimbali za utawala wakati washirika mbalimbali wanaposhiriki katika mfumo wa uhifadhi. Kwa mfano, mfumo wa kimataifa wa maeneo ya hifadhi unaojumuisha maeneo yanayotawaliwa na aina mbalimbali za washirika (kwa mfano., manispaa, mashirika binafsi, watu wa asili, vyama, mashirika yasiyo ya kiserikali, wizara na mashirika mbalimbali) chini ya mipangilio tofauti (kwa mfano, utawala shirikishi, usimamizi uliokasimishwa) ni tofauti zaidi kuliko mfumo ambao, tuseme, unajumuisha tu hifadhi za taifa zilizo chini ya wakala mmoja wa uhifadhi.

Mfumo wa vitengo mbalimbali vya eneo unaweza kubainishwa pia ndani ya eneo moja lililohifadhiwa, kama vile wakati eneo lilianzishwa kwa kuingiliana na maeneo ya hifadhi ya jadi yaliyokuwepo chini ya mamlaka yao ya utawala. Kutangaza na kutambua ushirikiano wa washirika mbalimbali wa utawala katika mwingiliano kama huo unaweza pia kuchukuliwa kama ‘kuimarisha aina mbalimbali za utawala’[9].

Mifumo iliyo na aina nyingi mbalimbali za utawala inahitaji juhudi za pamoja za utaratibu ili kuratibu washirika wote. Hata hivyo, za jumuishi zinachukuliwa kuwa halali zaidi. Kwa vile wanaweza kubuni na kutekeleza aina kubwa zaidi za ufumbuzi wa matatizo, unaoweza pia kuwa stahimilivu na endelevu.

Ubora wa utawala ni nini?

Tunazungumza kuhusu ubora wa utawala au ‘utawala bora’, iwapo maamuzi yanapofanywa huku yakiheshimu kanuni kadhaa zilizowekwa katika katiba, sheria, sera, desturi za kitamaduni na sheria za kimila za nchi fulani, na/au zilizokubaliwa kimataifa kama sehemu ya maamuzi ya kimataifa na mikataba. Kanuni za Umoja wa Uhifadhi wa Mazingira Kimataifa za utawala bora kwa maeneo yaliyohifadhiwa zinajumuisha: uhalali na sauti; mwelekeo; utendaji; uwazi; uwajibikaji; na usawa na kuheshimu haki.[10] ‘Ubora’ ni mali inayoweza kumaanisha usimamizi wa mfumo wa vitengo vya eneo, lakini mara nyingi humaanisha utawala wa eneo au maeneo.

Uhai wa utawala bora ni nini?

Hivi majuzi, majadiliano yamekwenda mbali zaidi ya aina mbalimbali za utawala bora ili kuangazia zaidi dhana ya uhai wa utawala.[11] Dhana hii ilianzishwa kama uwezo wa mpangilio wa utawala “kujifunza, kubadilika na kutimiza majukumu na wajibu kwa njia ambazo zinafaa kwa wakati, akili, zinazofaa na za kuridhisha kwa kila mtu anayehusika”.[12] Neno ‘uwezo wa kuishi linatokana na neno la Kilatini vita, ambalo linamaanisha uhai. Kwa njia fulani, inaunganisha wakala wa watu na wakala wa maumbile mengine (uhai wa maumbile yenyewe). Mfumo wa utawala ambao una uhai hudumisha utendakazi kupitia wakati na mabadiliko ya hali yenyewe. Ina stamina (uwezo wa kuendelea) na ni stahimilivu katika kukabiliana na matatizo na changamoto, lakini pia ni ya kutegemewa na inayofanya kazi, ikionyesha nia na uwezo wa kuchukua fursa katika muktadha wowote au mazingira fulani. Uthabiti wa utawala unaonekana wazi kama vile katika uwakala chanya-hatua inayochukuliwa kwa uhuru kuelekea malengo yenye maana na yenye kusudi. Hii, ikiwa ni lazima, hufikia uwezo wa mabadiliko.

Mfumo muhimu wa utawala huzalisha na kusambaza maarifa yanayohusiana na maamuzi ya hali halisi. Angalau aina mbili za maarifa zinaonekana kuwa za msingi kwa utawala wenye ufahamu wa kutosha kwa ajili ya uhifadhi: #maarifa ya jadi, wakati fulani hurithishwa miongoni mwa vizazi vilivyopita na maarifa yanayotokana na utafiti wenye malengo yanayofaa na uvumbuzi wa kiteknolojia (sio wa mwisho, njia za kisasa kama vile kupata taarifa za mahali kwa kupima kutoka kwenye satelaiti na kuangalia mabadiliko ya sura ya nchi).[13] Kutokana na ujuzi wa aina tofauti na asili, mfumo muhimu wa utawala huzuia matatizo na matishio na hupata manufaa kutokana na fursa. Hii ina maana kwamba una ufahamu wa kutosha, wa kutambua kuhusu maana na umuhimu wa aina mbalimbali za taarifa za kimkakati na kwa wakati unaofaa.

Zaidi ya hayo, mfumo wa utawala unaoonyesha uhai thabiti unahitaji kuwa na uwezo wa kubaki imara wakati wa malalamiko (kwa mfano, faida za muda mfupi, machaguo rahisi na wa ubinafsi, mambo ya ufisadi, n.k.) ambayo yanaweza kusababisha maafa baadaye. Kwa maneno mengine, maamuzi unayofanya yana maana na ni chanya kwa muda mrefu, kulingana na muktadha. Tafsiri ya hili inaonyesha kuwa uhai wa utawala lazima unatokana na mfumo wa miiko, au angalau mtazamo wa ulimwengu unaoweza kutokana na kutoa msukumo na mwongozo wa miiko kwa jamii kuhusu maamuzi yatakayofanywa kwa ajili ya eneo lililoko hatarini. Baadhi yetu humaanisha hili kama ‘thamani ya maisha’, ambapo maisha yanamaanisha mazingira na bioanuwai lakini pia kwa jamii kwa ujumla, na kuendelea kwa ustawi wa jamii hususani wamiliki husika.

Hatimaye, kipengele kingine cha uhai wa utawala ambacho kinaweza kisionekane mara moja na mara chache kiwepo kikamilifu, ni uwezo wa huruma na kujali. Mawakala wa maamuzi wenye ujuzi na maadili mema wanaweza kufanya kazi vizuri, lakini kuthamini kwa kina mazingira na watu huongeza kitu kisichoonekana lakini chenye nguvu sana kwa utashi wao na uwezo wa kuhifadhi mazingira kwa pamoja. Zaidi ya ‘kutawala eneo’, kuwa #wamiliki wake kunamaanisha kutunza na kukuza katika sehemu hiyo maalum uhusiano wa heshima na wa kudumu kati ya wanadamu na visivyo wanadamu – kitu ambacho ni sawa na muunganiko wa kitovu au hisia za upendo kuliko uhusiano wa kisayansi au kiuchumi. Ikichota kutoka kwa uwezo wake wa kufanya kazi, kuwa na uthabiti, utendaji, ubunifu, ufahamu wa kutosha, utambuzi, maana, thamani ya maisha na kujali, mfumo muhimu wa utawala una uwezekano wa kufanya uchaguzi mzuri, ambao utatoa matokeo chanya kwa mazingira na watu.[14] Kupitia hilo, unapaswa kupata kipimo cha uaminifu na heshima ya kijamii, mshikamano na msaada wa pamoja. Hata hivyo, kile ambacho kinaweza kuwa chanya ndani ya nchi kinaweza kisithaminiwe kwa kiwango tofauti katika eneo lingine, au kinyume chake. Ndiyo maana hata utawala ambao umepata nguvu ya kitaasisi katika ngazi fulani unahitaji kuilinda katika ngazi mbalimbali.


Rejea muhimu:

Graham, Amos na Plumtre na wenzake., 2003; Dudley (tafsiri), 2008; Borrini-Feyerabend na wenzake., 2013; Kituo cha Kimataifa cha Utawala wa Wenyeji, 2013; Almeida na wenzake., 2015; Borrini-Feyerabend na Hill, 2015; Mkataba kuhusu Bioanuwai, 2018a; Mkataba kuhusu Bioanuwai, 2018b.

Kwa mchanganyiko wa mashauriano ya haraka juu ya utawala wa maeneo yaliyohifadhiwa, tazama: Borrini-Feyerabend na wenzake, 2014. Tazama pia: Utawala kwa Uhifadhi wa Mazingira – filamu tatu fupi; Ukurasa wa Umoja wa Uhifadhi Mazingira Kimataifa kuhusu Utawala, usawa na haki


[1] Graham, Amos na Plumtre, 2003.

[2] Borrini-Feyerabend, na wenzake., 2013

[3] Borrini-Feyerabend na wenzake., 2014

[4] Mkataba kuhusu Bioanuwai, 2018b

[5] Almeida, 2015.

[6] Mkataba kuhusu Bioanuwai, 2018b

[7] Borrini-Feyerabend na wenzake., 2013, kama ilivyonukuliwa katika Mkataba kuhusu Bioanuwai, 2018b

[8] Kituo cha Kimataifa cha Utawala wa Wenyeji, 2013.

[9] Stan Stevens, mawasiliano binafsi, 2019.

[10] #Utawala na rejea zilizomo ndani yake.

[11] Majadiliano juu ya dhana hiyo yalianzishwa mwaka 2014 katika Mkutano wa Kimataifa kuhusu Hifadhi, Sydney (tazama Umoja wa Uhifadhi wa Mazingira Kimataifa, 2014 na Borrini-Feyerabend na wenzake., 2014). Kitini cha Muhtasari uliokusudiwa kwa uhai wa utawala kwa maeneo yaliyohifadhiwa ambacho kinatayarishwa kwa sasa.

[12] Borrini-Feyerabend na Hill, 2015, ukurasa wa 192 na kurasa zinazofuata.

[13] Hili ni wazi kuwa ni jambo la msingi kuhusu mabadiliko ya tabianchi na athari nyingine za mabadiliko kimataifa, na kwa ajili hiyo uhai wa utawala unahitaji ufuatiliaji endelevu, marekebisho, na kukusanya taarifa kwa ajili ya mipango na hatua za muda mfupi na mrefu, pia hekima na uwezo wa kufanya kazi na jamii ili kusaidia maamuzi na kutekeleza hatua za kukabiliana na hali hiyo.

[14] Angalau kwa muda mrefu, wakati kujitoa kwa haraka ni muhimu kufikia malengo ya muda mrefu.